Index   1  2  3  4  5  6  7  8  9  10  11  12  13  14  15  16  17  18  19  20  21  22  23  24  25  26  27  28  29  30  31  32  33  34  35  36  37  38  39  40  41  42  43  44  45  46  47  48  49  50  51  52  53  54  55  56  57  58  59  60  61  62  [63]  64  65  66  67  68  69  70  71  72  73  74  75  76  77  78  79  80  81  82  83  84  85  86  87  88  89  90  91  92  93  94  95  96  97  98  99  100  101  102  103  104  105  106  107  108  109  110  111  112  113  114 
AL MUNAAFIQUUN

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

[63.1] Wanapo kujia wanaafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanaafiki ni waongo.

[63.2] Wamevifanya viapo vyao ni kinga, na wao wakajizuia kuifuata Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika ni mabaya kabisa waliyo kuwa wakiyafanya.

[63.3] Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha wakakufuru; kwa hivyo umepigwa muhuri juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo hawafahamu lolote.

[63.4] Na unapo waona, miili yao inakupendeza, na wakisema, unasikiliza usemi wao. Lakini wao ni kama magogo yaliyo egemezwa. Wao hudhania kila ukelele unao pigwa ni kwa ajili yao. Hao ni maadui; tahadhari nao. Mwenyezi Mungu awaangamizilie mbali! Vipi wanapotoka na haki?

[63.5] Na wanapo ambiwa: Njooni ili Mtume wa Mwenyezi Mungu akuombeeni maghfira, huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wanageuka nao wamejaa kiburi.

[63.6] Sawa sawa kwao, ukiwatakia maghfira au hukuwatakia maghfira, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.

[63.7] Hao ndio wanao sema: Msitoe mali kwa ajili ya walioko kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ili waondokelee mbali! Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye khazina za mbingu na ardhi, lakini wanaafiki hawafahamu.

[63.8] Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui.

[63.9] Enyi mlio amini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio walio khasiri.

[63.10] Na toeni katika tulicho kupeni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti, tena hapo akasema: Mola wangu Mlezi! Huniakhirishi muda kidogo nipate kutoa sadaka, na niwe katika watu wema?

[63.11] Wala Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote inapo fika ajali yake; na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.